MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani Kilimanjaro, imewaachia huru washtakiwa watano kati ya 12 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya wizi wa zaidi ya shilingi million 239 mali ya benki ya NMB tawi la Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya kubaini kuwa hawana hatia.
Pamoja na kuachia huko,lakini washtakiwa hao bado wataendela kusota rumande kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya mauaji ya askari polisi mwenye namba Ex E.6825 PC Michael Milanzi aliyekuwa lindoni siku ya tukio la uporaji ndani ya benki hiyo,ambapo kesi hiyo nasubiri kuhamishiwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kilimanjaro.
Washtakiwa walioachiwa ni Deodat William Temu (39),Emmanuel Eliaza Mziray (36),Florian Anthony Kimati (37),askari aliyewahi kuwa lindoni kwenye benki hiyo mwenye namba 940 PC Nathaniel Manyama na aliyekuwa mhasibu wa benki hiyo Salome Matemu.
Washtakiwa hao ni mshtakiwa wa tano,sita ,saba na wanane ambao walikuwa wakitetewa na wakili maarufu jijini Arusha Mediam Mwale akisaidiana na wakili Andrew Maganga huku mshtakiwa Matemu akitetewa na wakili John Ruwaichi.
Washtakiwa ambao wamekutwa na hatia na hivyo watakuwa na kesi ya kujibu ni mshitakiwa wa kwanza Samwel Gitau Saitoti maarufu kama Saimoo (33),mshtakiwa wa pili Michael Kimani Peter maarufu kama Kimm (40) raia wa Kenya,mshtakiwa wa wa tatu Calist Joseph Kamili Kisambu Kanje (47) ambao wanatetewa na wakili Mwale.
Wengine ni mshtakiwa wa nane Devotha Elias Msanze (35),mshtakiwa wa tisa ,Juliana Elias Msanze (45),mshtakiwa wa kumi Elizabeth Elias Msanze (24) na mshtakiwa wa 11,Ntabasile Elias Msanze ambao ni ndugu kwa maana ya mama na watoto wake na ambao wanatetewa na wakili Ruwaichi.
Akisoma hukumu hiyo iliyochukua takribani dakika tano,kwa niaba ya jopo la mahakimu watatu,Penterin Kente,Aziza Temu na John Nkwabi,Kente alisema mahakama hiyo imesikiliza ushahidi ulitolewa mahakamani humo na jumla ya mashahidi 19 wa upande wa mashtaka na kupokea hoja za mawakili wa pande zote mbili kwa njia ya maandishi na kujirisha na kisha kutoa maamuzi.
“Baada ya kupitia kwa kina mahakama imeona kabisa ushahidi unatosha kuwatia hatiani washtakiwa saba ,washtakiwa watano mahakama imeshindwa kuwatia hatiani kwa kuwa ushahidi uliotolewa mahakamani haujawagusa na kama umewagusa ni kidogo sana na hata mahakama ikiendelea kuwabakisha hawatakutwa na hatia yoyote”alisema Kente.
Alisema msimamo wa kuonyesha washtakiwa hao hawana hatia umeanza tangu kwenye hoja za upande wa mashtaka na mashahidi walioletwa kwani hata kama hawakueleza wazi lakini washtakiwa hao hawana kesi ya kujibu.
“Kwa mujibu wa kifungu namba 230 cha sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002,mahakama hiyo imetupilia mbali mashtaka dhidi ya washtakiwa hao,kama hamna sababu yoyote ya kuendelea kuwashikilia basi waachiwe huru”alisema
Hata hivyo,alisema mahakama hiyo inatambua kuwa washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi nyingine ya mauaji hivyo kuachiwa kwao huru kutategemeana na kumalizika kwa kesi hiyo nyingine ambayo inasubiri kuhamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania kwa kuwa mahakama hiyo haina nguvu ya kisheria ya kusikiliza kesi hiyo.
Aidha,mahakama hiyo ilihairisha kesi hiyo na ile ya mauaji inayotajwa mbele ya Hakimu Nkwabi hadi Desemba 06 mwaka huu,ambapo washtakiwa hao watapewa nafasi ya kuchagua namna ya kujitetea kama ni kwa njia ya kiapo kwa kuleta mashahidi wao au la.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kula njama na wizi wa kutumia silaha kinyume na sheria,ambapo pia washtakiwa wengine wawili wameunganishwa kwenye kesi ya mauaji na kufanya jumla yao kuwa 14.
Mara baada ya kutolewa uamuzi huo ndugu,jamaa na marafiki wa washtakiwa hao waliokuwa wamejitokeza kwa wingi mahakamani humo, pamoja na washtakiwa wanaoendelea kung’ang’aniwa,walionekana wakiwa na nyuso za simanzi na huzuni kwani wengi walikuja kwa matumaini ya kuondoka na ndugu zao.
Tukio la uporaji ndani ya benki hiyo,lilitokea Julai 11 mwaka huu,majira ya saa 1:30 usiku,ambapo kundi la watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi walivamia na kupora kiasi hicho cha fedha na kisha kutokomea nacho kusikojulikana na kumuua askari mmoja aliyekuwa lindoni na kumjeruhi mwingine.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment